Viongozi wa Upinzani wakamatwa kwa kushinikiza maandamano


 Baadhi ya viongozi wa upinzani nchini Tanzania wanashikiliwa na polisi baada ya kutangaza kupanga maandamano ya amani siku ya Jumatatu ili kuonesha kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi.

Polisi wanasema wamemkamata mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Chadema bwana Freeman Mbowe pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es Salaam Boniface Jacob.

Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema walipiga marufuku maandamano hayo yaliyopangwa kuanza leo asubuhi, lakini viongozi wa Chadema "wameonekana kufanya vikao kuratibu maandamano ya fujo".

Amesema viongozi hayo walipanga kuhatarisha usalama wa raia kwa kwa kufanya vurugu kuonyesha kutokubaliana na matokeo, watu hao wanapanga kuingia mtaani kuchoma maeneo mbalimbali kama masoko, magari na vituo vya mafuta.

Aidha amesisitiza kuwa operesheni kubwa inaendelea kwa yeyote ambaye atashiriki kuratibu, kuwezesha au kushiriki katika maandamano hayo atafikishwa kwenye mikono ya sheria.

Baada ya rais John Magufuli kutangazwa kuwa rais kwa awamu ya pili siku ya Ijumaa usiku, viongozi wa vyama vikuu vya upinzani nchini Tanzania walitangaza kutokubaliana na matokeo hayo na kuitisha maandamano leo hii.

CHADEMA

Vyama vikuu vya upinzani nchini Tanzania Chadema na ACT-Wazalendo vinataka kurejewa kwa Uchaguzi Mkuu nchini humo.

Vyama hivyo viwili vinapinga matokeo ya uchaguzi wa Jumatano ambapo rais aliye madarakani John Magufuli amekwishatangazwa mshindi.

Katika mkutano wa wanahabari wa pamoja baina ya viongozi wa Chadema na ACT Wazalendo vyama hivyo pia vimeitisha maandamano ya nchi nzima ili kudai kurejewa kwa uchaguzi huo.

Maelezo ya video,

Matokeo ya uchaguzi Tanzania 2020: Kauli ya vyama vya upinzani

Mwenyekitiwa Chadema Taifa Freeman Mbowe ameeleza kuwa: ''kilochofanyika si uchaguzi ni unyang'anyi wa demokrasia uliofanywa na ZEC (Tume ya Uchaguzi Zanzibar) na NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) .

Vyama hivyo sasa vinataka kuvunjwa kwa Tume ya NEC na ZEC.

Vyama hivyo aidha vimewaomba Watanzania kufanya maandamano ya amani.

''Kuanzia Jumatatu, wanachama wa vyama vyetu na wote wasiokubaliana kushiriki katika maandamano ya amani kuanzia Novemba 2 hadi hapo madai yetu yakapotelekezwa'' walisema.

Siku ya Alhamisi Mwenyekiti wa ACT Wazalendo ambaye pia alikuwa mgombea wa urais visiwani Zanzibar, Maalim Seif Seif Sharif Hamad alikamatwa pamoja na viongozi wengine wa chama hicho.

Kamanda wa Polisi Mjini Magharibi Zanzibar Awadhi Juma alisema Maalim Seif alikamatwa akiwa anafanya maandamano ambayo hayana kibali akiwa na wafuasi wa chama chake.

No comments