Ticker

6/recent/ticker-posts

Advertisement

Zuchu Apata Pigo Zito


 DAR ES SALAAM: Mtihani mzito! Staa wa Bongo Fleva, Zuhura Othman ‘Zuchu’ amepata pigo la aina yake kufuatia baba yake mzazi Othman Soud kupata ugonjwa wa kupooza ghafla, RISASI linakupa habari kamili.

Taarifa kutoka nyumbani kwa mzee huyo, Zanzibar zimeeleza kuwa, mzee huyo alipata tatizo hilo la kupooza kuanzia kiunoni mpaka chini.

“Huu ni mtihani mzito kwa kweli, unajua kupooza sio ugonjwa wa kupona leo au kesho. Sasa hivi ndio hivyo tena mzee wetu amepooza,” alieleza mmoja wa wanafamilia ambaye hakupenda jina lake lichorwe gazetini.

RISASI LAMTAFUTA

Baada ya kuelezwa habari hiyo, RISASI JUMAMOSI lilifanya jitihada za kumtafuta mzee huyo kwa njia ya simu na kufanikiwa kuzungumza naye huku akionesha sauti ya huzuni.

HUYU HAPA TUMSIKIE…

Akizungumza na RISASI JUMAMOSI, baba Zuchu alisema alipatwa ugonjwa huo wa kupooza ghafla akiwa kwenye mizunguko yake ya kutafuta riziki na kwamba bado anapatiwa tiba ya maradhi yake hayo.

“Nilikuwa vizuri tu lakini wakati nikiwa kwenye mizunguko yangu nikaanza kuhisi hali ya mwili wangu tofauti, mara ghafla nikapatwa na ugonjwa huu wa kupooza kuanzia kiunoni hivyo siwezi kukaa wala kutembea na kuendelea na shughuli zangu kama ilivyokuwa zamani,” alisema baba huyo.

AMZUNGUMZIA ZUCHU

Baba wa mwanamuziki huyo alisema, pia pamoja na kupata mtihani huo lakini anamshukuru mtoto wake kuwa pamoja naye na hata kuja kumuona kwakwe ni faraja kubwa.

“Naumwa lakini nafarijika sana kuonana na mwanangu na kuja kunitembelea ni jambo muhimu sana kwangu na ninachokiamini nitapona tu na kuendelea na kazi zangu kama kawaida,” alisema baba huyo ambaye naye alikuwa mwanamuziki mahiri wa Taarab, bara na visiwani.

TUJIKUMBUSHE KIDOGO

Kabla ya baba Zuchu hajaibuliwa na magazeti ya Global Publisher, kulikuwa na maswali ya watu wengi kutaka kujua mahali alipo mzazi huyo ambapo pia yalizungumzwa mengi kwenye mitandao ya kijamii.

Kuna ambao walisema Zuchu na baba yake huyo ana ugomvi mzito lakini hata hivyo, baada ya gazeti la IJUMAA WIKIENDA kuandika habari ya mzazi huyo kwa mara ya kwanza, Zuchu alitimba visiwani Zanzibar na kukutana na mzazi wake kisha akashea picha ya pamoja kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Zuchu alisindikiza picha hiyo aliyokuwa na baba yake kwa ujumbe huu:

“Is officially my favorite year BABAANGU. Allah atuweke karibu leo mpaka milele. Amani ninayoishi hakuna anaeelewa jinsi ninavyojisikia. Yaliyopita yamepita Allah atuongoze kwenye yajayo I’m so happy.”

HAWAKUWA SAWA

Kabla ya Zuchu kupiga picha ya pamoja na baba yake huyo, ni miaka mingi ilipita bila wawili hao kuwa pamoja huku ikielezwa kwamba, hawakuwa kwenye mawasiliano mazuri.

Hata hivyo, baada ya kuandika ujumbe huo ni dhahiri alionesha sasa wapo kwenye ukurasa mpya wa maisha hivyo mrembo huyo anayetamba na wimbo wa No Body aliomshirikisha staa wa Nigeria Joeboy anao wajibu wa kumhudumia kwa karibu mzazi wake.

Post a Comment

0 Comments