Ticker

6/recent/ticker-posts

Advertisement

Wanawake Wadai Kubakwa na Askari Bila Kinga


 HAKIYANANI; dunia ina vioja vingi! Baadhi ya wanawake jijini Dar es Salaam wameibua madai mazito kwamba wanabakwa usiku wa manane na askari tena bila kinga. Wanawake hao bila kupepesa macho mwishoni mwa wiki iliyopita waandishi wetu waliowaita ili wawape ushauri wa hatua gani za kuchukua:

 

“Sisi ni wanawake, tuna familia zetu, tunaendesha maisha yetu kwa kufanya biashara ya kuuza miili yetu, hili hatutaki kuficha.

“Kinacho tusikisha, tukiwa kwenye kazi zetu askari wanatukamata na kutufanyia udhalilishaji mkubwa wa kijinsia,” alisema mmoja wa wanawake hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Husna ambaye amedai kufanya kazi hiyo haramu maeneo ya Sinza, Dar.

 

SIMULIZI NAMNA WANAVYOBAKWA

Aidha, Husna huku akiungwa mkono na wenzake aliendelea kudai kuwa mara kadhaa wamekuwa wakikamatwa na kuishia kubakwa na askari bila kupewa chochote kisha kuachiwa.

Akielezea mazingira ya kubakwa kwao mwanamke huyo alisema askari hao wanapowakamata huwaweka kwenye magari kwa madai ya kupelekwa vituo vya polisi lakini huishia kuingizwa vichochoroni ambako hulazimishwa kufanya ngono na askari tena bila kutumia kinga.

 

WAHOFIA MAGONJWA

“Pamoja na kazi yetu ya kujiuza sisi tuko makini na afya zetu, tunatumia kinga, lakini hawa askari huwa hawataki kuvaa kondomu.

“Hii inatuweka kwenye mazingira magumu ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa ukiwemo Ukimwi. “Mbali na huo unyama wanaotufanyia hao askari wakati mwingine wakimaliza kukubaka wanakusachi hela ulizonazo, wanachukua,” alisema mwanamke mwingine aliyegoma kutajwa jina lake kwa madai kuwa anafahamika na wengi.

 

WAOGOPA KURIPOTI POLISI

Akijibu swali la mwandishi wetu kuwa kwa nini huwa hawaripoti polisi vitendo hivyo vya ubakaji wanavyofanyiwa na watu waliowaita askari mwanamke mingine aliyejiita jina la Agness alisema: “Unafanya biashara ya bangi halafu unajipeleka kituoni kulia umedhurumiwa.

“Biashara ya ukahaba haikubaliki hapa nchini, unakwendaje kuripoti polisi kuwa umedhalilishwa kingono?”

 

WAILILIA SERIKALI

Katika hatua nyingine wanawake hao wanaofanya baishara ya kuuza miili yao wameiomba serikali kupitia kwa Waziri wa Sheria na Katiba, Mwigulu Nchemba wawaruhusu kufanya biashara hiyo kwa kuwa si kosa la jinai.

 

“Mimi nimekamatwa zaidi ya mara ishirini, lakini ukikamatwa kinatokea nini, unapelekwa Mahakama ya Jiji huko unashtakiwa kwa kosa la uzembe na uzururaji.

 

“Kosa la nini? Uzembe na uzururaji siyo ukahaba; hii maana yake ni kwamba hakuna kosa la mtu kuuza mwili wake. “Siku hizi wanawake wengi tu wanajiuza, sema wao wanaonekana tofauti na sisi kwa sababu wanakodi vyumba vya hoteli na sisi tunasimama mabarabarani lakini wote tunafanya kazi moja.

 

“Mi naomba serikali, naliomba jeshi la polisi chini ya IGP Simon Sirro waache kutunyanyasa sisi wanawake kwa sababu kama ni biashara tunayoifanya hatuwezi kuifanya kama wateja wa kiume hawapo, mbona wao hawadhalilishwi?”

 

WALIA BIASHARA NGUMU

Mbali na malalamiko hayo ya kudhalilishwa kingono wanayodai, wanawake hao ambao wanafanya biashara ya kuuza miili yao maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, wamelia kuwa kwa sasa biashara hiyo ni ngumu. Walisema imewalazimu kupunguza bei kutoka elfu kumi waliyokuwa wanatoza mwanzo hadi shilingi elfu tano kutokana na watu kukosa fedha.

 

“Siku hizi hakuna hela, zamani tulikuwa tunapiga hela nyingi siku hizi wanaume wanalialia tu, wakati mwingine hata elfu tatu unachukua.

 

“Hii biashara ni ngumu, kutokana na hali ilivyo unaweza kukuta mwanaume anataka huduma yako, unamwambia mfano elfu tano anakupa.

 

“Mkifika eneo la tukio akimaliza shida zake anaanzisha ugomvi ili nini achukue ile hela awe ameburudika bure, sasa hapo ndiyo inabidi upambane kivyako.

 

“Maana huwezi kusema utampeleka polisi mtakamatwa wote, inabidi kama noma iwe noma ili nini upate haki yako maisha yasonge,” alisema mwanamke mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Aziza.

 

KAMANDA WA POLISI AFUNGUKA

Mwandishi wetu alizungumza na Kamanda wa mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi (ACP) Edward Bukombe ambaye alifunguka kuhusiana na tuhuma hizo kama ifuatavyo:

 

“Hilo suala ndiyo kwanza nalisikia lakini kama kweli lipo bado halijanifikia mezani kwangu na kama halijanifikia hatuwezi kushughulikia tetesi waje wafungue kesi tutawasikiliza. “Waje tu tutalishughulikia tatizo lao wasiishie kulalamikia huku mitaani haitawasaidia kitu.”

 

MWANASHERIA AFUNGUKA

Mwanasheria wa kujitegemea Emmanuel Elius wa Mikocheni jijini Dar alipozungumza na waandishi wetu kuhusiana na sakata la madai ya wanawake hao kubakwa na hatua za kisheria za kuchukua alisema:

 

“Hawapaswi kuogopa kwenda kuripoti kituo cha polisi kwa sababu hata kama ni wahalifu kwa namna moja lakini hakuna uhalali unaompa mtu mwingine awe polisi au askari yeyote kumfanyia jinai mtu kwa sababu anatuhumiwa kwa uhalifu.

 

“Wao wanapashwa kupeleka malalamiko yao polisi wakiwa na ushahidi wa kubakwa kwao na ikithibitika askari waliofanya kosa hilo wanahukumiwa kwa kufanya kosa la jinai.”

 

Hata hivyo, mwanasheria huyo aliwashauri wanawake wanaotumia miili yao kupata fedha waache kufanya hivyo kwa sababu licha ya kuwa sheria hailizungumzii suala la uchagudoa kuwa ni kosa lakini kijamii siyo jambo zuri kufanywa. Alisema, yapo mambo ambayo yanaweza kuwa siyo makosa kisheria lakini kijamii yakamshushia mtu heshima yake.

Post a Comment

0 Comments