Upinzani wadai watu 8 wameuawa Zanzibar, polisi yakanusha

 

Watu wanane wanadaiwa kuuawa katika visiwani Zanzibar kufuatia ghasia za uchaguzi, kinaripoti chama kikuu cha upinzania visiwa humo, madai ambayo hata hivyo yamekanushwa na polisi.

Kulingana na taarifa zilizotolewa na chama cha upinzani cha ACT Wazalendo watu hao wameuawa katika kisiwa cha pemba kwa silaha za moto.

Ripoti za awali zilizoanza kusambaa mtandaoni usiku wa jana zilidai kwamba usiku huo wa kuamkia leo Jumanne Oktoba 27 watu watatu waliuawa kwa risasi, lakini kutoka asubuhi ya leo idadi ya wanaoripotiwa kuuawa visiwani humo imeongezeka mpaka kufikia watu wanane.

Je polisi inasema nini

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania IGP Simon Sirro amekanusha kutokea mauaji na badala yake amesema jeshi hilo limewakamata vijana 42 kutokana na ghasia zilizoshuhudiwa Pemba hapo jana

IGP Sirro amesema kwamba wale waliokamatwa ni vijana waliokuwa wakirushia mawe maafisa wa polisi waliokuwa katika zamu pamoja na maafisa wa kusimamia uchaguzi waliokuwa zamu wakisambaza vifaa vya kupigia kura kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa leo.

Sirro pia alitoa onyo kwa watu binafsi na makundi ya watu wanaopanga kusalia katika vituo vya kupigia kura baada ya kupiga kura akisema hilo halitakubalika.

IGP Sirro amesema kwamba shughuli ya kulinda kura itafanywa na mawakala wa vyama husika.

''Kupiga kura , kuhesabiwa kura na kutangazwa kwa matokeo , hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi bila hofu yoyote. Baada ya kupiga kura warejee majumbani na kwenye shughuli zao''.

Aidha amewataka raia kutoshawishiwa au kujiingiza katika vurugu za aina yoyote zitakazozua vurugu.

Unaweza kutazama

Maelezo ya video,

Siro:Tutasimamia haki,viongozi wa kisiasa watimize wajibu wao

''Endapo kuna malalamiko ya aina yoyote taratibu zilizoelekezwa na sheria zifuatwe na siyo kujichukulia sheria mikononi kwa kuleta vurugu au fujo'', ilisema taarifa hiyo.

Awali, Kamishna Msaidizi wa polisi kisiwani Pemba Juma Saad Hamis pia alikanusha kutokea mauaji akiiambia BBC kwamba polisi walitumia vitoa machozi pekee na si risasi za moto.

No comments