Ubalozi wa Marekani wataka kero za uchaguzi kushughulikiwa


 Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umezitaka mamlaka za taifa hilo la afrika mashariki kushirikiana na wadau mbalimbali kushughulikia kwa uwazi malalamiko yanayotolewa kuhusu uchaguzi mkuu uliofanyika oktoba 28 mwaka huu.

Ubalozi huyo kupitia tamko lake lililotolewa oktoba 29, mwaka huu unasema kufanya hivyo kutarejesha imani na kutekeleza azma ya kuheshimu utawala wa sheria na dhana ya utawala bora.

Moja ya malalamiko yaliyotajwa na ubalozi huyo ni kuhusu uwepo wa kura feki katika uchaguzi huo ambao, matokeo yake yanaendelea kutolewa.

Malalamiko hayo yalishatolewa ufafanuzi na kupingwa na Tume ya taifa ya uchaguzi kwamba hayana ukweli kupitia kwa mwenyekiti wake, Jaji Kaijage.

''Kuna taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kuwepo kwa masanduku ya kura feki katika majimbo ya Kawe Dar es Salaam, Pangani Tanga na Buhigwe Kigoma',' alisema Bw. Kaijage.

Aliongeza kuwa taarifa ya madai hayo jumla na ambayo sio rasmi hayajathibitishwa na hayaelezi ni vituo vipi vinahusika na matokeo hayo

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema haijapokea taarifa ya madai hayo.

Ubalozi wa Marekani pia ulilalamikia hatua ya kukamatwa kwa kiongozi wa upinzani Visiwani Zanzibar Maalim Seif Hammad.

Katika ujumbe wa Twitter Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald J Wright, alisema kuwaweka kizuizini viongozi wa upinzani sio kitendo cha serikali kujiamini katika ushindi wake wa uchaguzi, kutaka kuachiliwa kwa mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Maalim Seifa na viongozi wengine.

Ruka Twitter ujumbe, 1

Mwisho wa Twitter ujumbe, 1

Maalim Seif tayari ameachiliwa kwa dhamana.

Mwanzoni mwa mwezi Oktoba Ubalozi wa Marekani ulisema kwamba haumuungi mkono mgombea yeyote au chama chochote katika uchaguzi wa Tanzania.

Kupitia taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya ubalozi wa taifa hilo nchini Tanzania, ubalozi huo hatahivyo ulimesema kwamba utafuatilia kwa karibu matendo ya watu wanaoingilia na kuvuruga mchakato wa kidemokrasia au kuchochea vurugu dhidi ya raia.

Aidha ubalozi huo pia ulisema unaunga mkono wito uliotolewa na wagombea wakuu wa kuwepo kwa mchakato wa uchaguzi wa amani na wenye uwazi.

''Tunatoa wito kwao na kwa wafuasi wao kuchukua hatua kutanzua hali ya usalama inayojengeka na kuepuka matamshi ya kichochezi'', ilionya taarifa hiyo.

No comments