NEC: Kura za Urais Zitahesabiwa Dar, Si Dodoma


 TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imevitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu kuhakikisha leo Oktoba 21, 2020, vinakabidhi orodha ya mawakala wa vyama vyao kwa wasimamizi wa uchaguzi.

 

Hilo limewekwa wazi na Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage, baada ya kumaliza siku ya kwanza ya mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu namna ya kuhabarisha masuala ya uchaguzi.

 

”Vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu vinatakiwa kuhakikisha Jumatano Oktoba 21, 2020, vinakabidhi orodha ya mawakala wa vyama vyao kwa wasimamizi wa uchaguzi kote nchini,” alisema Kaijage.

Katika hatua nyingine Kaijage aliweka wazi kuwa majumuisho ya kura zote za urais katika uchaguzi wa Oktoba 28, 2020 yatafanyika Dar es Salaam na si Dodoma ambapo ndipo yalipo makao makuu ya tume hiyo kwenye jengo la Uchaguzi House kama ambavyo imekuwa ikidaiwa.

 

Mafunzo kwa waandishi wa habari yanaendelea leo Jumatano, Oktoba 21, 2020 jijini Dar es Salaam.

No comments