Mobeto Ampigia Goti Zari!


 KUKUBALI yaishe ni sehemu ya uungwana; ndivyo alivyofanya msanii wa Bongo Fleva na Mwanamitindo, Hamisa Mobeto ambaye amemtaka mwanamke mwenzake Zarinah Hassani ‘Zari’ kuweka kando tofauti zao ili maisha yaendelee.

 

Hamisa na Zari ni wazazi wenzake na msanii maarufu wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘ Diamond’, wamekuwa katika bifu la chini kwa chini kwa muda mrefu lisilokuwa na kichwa wala miguu.

 

Akizungumza na AMANI Mtandaoni, Hamisa alisema kuwa hana tatizo na Zari, kwa sababu wao ni ndugu kupitia kwa watoto waliozaa na Diamond.

 

“Sidhani kama nina tatizo kubwa na Zari na wala hatujawahi kugombana hata kidogo, ninachojua ni kwamba watoto wetu ni ndugu. “Kuna siku wanakaa pamoja na kufanya vitu vingi wakiwa ndugu au watakutana kwa baba yao sasa sisi kama wazazi wa kike tutengane kwa sababu gani?” alisema Mobeto.

 

Kauli hiyo ya Mobeto inakuja nyuma ya tetesi kuwa mwanamitindo huyo na Zari hawapikwi chungu kimoja kutokana na madai kuwa ndiye anayetajwa kuuvunja uhusiano wa Zari na Diamond.

 

Inafahamika kuwa wakati Zari akiwa anaishi Madale jijini Dar es Salaam na Diamond kama mke na mume, Diamond alikuwa akichepuka na mwanamitindo huyo kwa siri.

 

Kitendo hicho kiliwahi kutajwa na Zari kuwa miongoni mwa mambo yaliyomfanya afungashe virago na kurejea kwao Uganda huku akimtuhumu Diamond kuwa hakuwa mwaminifu kwenye penzi lao. Mobeto amezaa na Diamond mtoto mmoja wa kiume na Zari akibahatika kupata watoto wawili na msanii huyo nguli Bongo, mmoja akiwa wa kiume.

 

Huwenda kauli ya Mobeto kumtaka Zari tofauti zao ziishe ikafungua ukurasa mpya kwao na kuwafanya kuwa kitu kimoja.

 

Mara zote Diamond amekuwa akijiweka kando na mgogoro wowote unaowahusu wazazi wenzake na hajawahi kuonesha kumuunga mkono yeyote kwenye ugomvi wao ingawa mara kadhaa amekuwa akijitokeza kwenye vyombo vya habari na kuonesha ukaribu wake na Mobeto.

 

Aidha, msanii huyo amekuwa akionesha mahaba yake na Zari kwa kile anachodai kuwa ni mama wa watoto wake ambaye hastahili kujitenga naye mazima.

No comments