Maua Sama; Mgonjwa wa Hip Hop!

Maua Sama; Mgonjwa wa Hip Hop!


 

HUWEZI kukamilisha orodha ya wasanii wa kike wanaofanya vizuri Bongo, halafu jina la Maua Sama likawa halijaingia kwenye orodha yako.

Hauwezi kuacha kumtaja msanii huyu kwani, ameweza kujitengenezea jina kwa kuachia mikwaju mikali kama vile Niteke, Nioneshe na Iokote.

 

Risasi limeweza kufanya mahojiano maalum (exclusive interview) na Maua Sama ambapo amefunguka mengi, karibu:

RISASI: Unazungumziaje mafanikio yako tangu umeanza muziki wewe kama msanii?

 

MAUA SAMA: Kiukweli namshukuru Mungu tangu nianze muziki mpaka sasa, umenisaidia kwa sababu nimepiga hatua, ila bado sijafikia ninapopataka na nipo kwa ajili ya burudani zaidi.

RISASI: Kipindi cha nyuma ulifanya kazi na (ROSTAM), yaani Roma na Stamina na mlitoa ngoma ilibamba ambayo ni Kibamia, mbona ni muda mrefu umepita hatujaona ukifanya nao kazi tena?

 

MAUA SAMA: Unajua kila kitu kinaenda na wakati, pia unakuta kila mtu ana kazi zake, pia kama sasa hivi Roma hayupo kasafiri. Kwa hiyo, naweza nikasema muda wa kufanya kazi ukifika, tutafanya kazi tena.

RISASI: Tangu uanze muziki mpaka sasa, ni changamoto gani ulipitia au unaipitia?

 

MAUA SAMA: Kila safari ambayo ina mafanikio, ina changamoto hususan sisi watoto wa kike ni tofauti na wenzetu. Kama changamoto zipo, ni nyingi na siwezi kuzisema, maana hazitaisha ila mimi nazifurahia. Kiukweli siwezi sema nazikataa kwa sababu kupitia changamoto, zimeweza kunijenga kimaisha mpaka sasa.

 

RISASI: Unamzungumziaje Zuchu msanii wa kike mpya ambaye ameingia kwenye gemu hivi karibuni na anaonekana anafanya vizuri?

MAUA SAMA: Ni msichana ambaye kiukweli anajitahidi na kazi zake na anafanya vizuri na aendelee kumuomba Mungu afikie malengo yake pale ambapo anapataka yeye.

 

RISASI: Tuzungumzie huu wimbo wako mpya wa Kan Dance, kwa nini uliamua kuuita hilo jina na ukaamua kuliandika kama Kiswahili likiwa lina maana ya Kiingereza?

MAUA SAMA: Niliamua kuuita huu wimbo hivyo kwa sababu, niliona ni kitu kizuri, pia kama msanii unatakiwa kuwa mbunifu na kutengeneza kitu cha tofauti na nikaona kinafaa.

 

RISASI: Ulitoa wapi wazo la muziki wako wa Kan Dance au ni wazo ulipewa na mtu?

MAUA SAMA: Ni wazo ambalo nililipata studio na watu ambao tulikuwa wote mahala hapo, tukaona ngoja tufanye hiki kitu kwa pamoja na tukaona ni kitu cha tofauti na kitafaa pia.

 

RISASI: Kwa nini hukuamua kumshirikisha mtu kwenye wimbo wako huo mpya?

MAUA SAMA: Hili wazo ni la kwangu, tulishirikiana kwa pamoja lakini huu wimbo ilitakiwa niimbe mimi peke yangu nisishirikishe mtu, wao walinisaidia tu kwenye kuandika na mambo mengine, ila tumetengeneza kitu kizuri kiukweli namshukuru Mungu kwa hilo.

 

RISASI: Ni msanii gani unamkubali kwenye Bongo Fleva?

MAUA SAMA: Msanii wa Bongo Fleva ambaye namkubali kwanza; najikubali mimi mwenyewe kwa sababu natoa nyimbo kali, pia nashukuru Mungu Watanzania wananiunga mkono ila pia namkubali kaka yangu MwanaFA, basi!

RISASI: Ni wimbo gani katika nyimbo zako unaipenda sana?

 

MAUA SAMA: Napenda Kan Dance na si kwamba naupenda tu kwa sababu ni wimbo mpya, hapana ila naupenda pia kwa sababu hata ndugu zangu na watu wangu wa karibu wameukubali.

RISASI: Tumeona baba na mama yako wakicheza huu wimbo wakijirekodi, wewe kama mtoto wao unajisikiaje?

 

MAUA SAMA: Najisikia vizuri sana, ni furaha pia kuona hata wazazi wangu wanaunga mkono kazi yangu, kiukweli nafurahi sana sina neno lingine la kusema.

RISASI: Unapenda kufanya muziki wa pamoja na msanii gani hapa Bongo?

 

MAUA SAMA: Mimi kwanza napenda wasanii wanaofanya Hip Hop kwa sababu inaniongezea mzuka wa kufanya kazi, msanii kama G Nako, Darassa na hata Joh Makini, pia napenda kufanya nao muziki, yaani haijalishi ila napenda muziki wa Hip Hop.

RISASI: Ni vitu gani ambavyo Maua anafanya akiwa tofauti na muziki kwa muda huo?

 

MAUA SAMA: Mimi napenda kukaa nyumbani kiukweli, kwa sababu naona ni sehemu nzuri ya kutulia na kufanya mambo yangu ya msingi.

RISASI: Kuna biashara au kitu kingine unachofanya tofauti na muziki?

 

MAUA SAMA: Ndiyo sisi kwetu tunalima, tuna mashamba ambayo tunalima. Silimi mimi, ila kuna watu ambao tunafanya nao hicho kilimo, mimi na wazazi wangu.

RISASI: Unazungumziaje mahusiano yako? Na je, ni kitu gani uliwahi kukifanya kwenye mapenzi unakijutia mpaka leo?

 

MAUA SAMA: Kwanza mahusiano yangu yapo tu vizuri sina shida yoyote ile, pia katika mapenzi sijawahi kujuta na sijawahi kukutwa na tukio kubwa la kusema litanifanya nijute.

RISASI: Asante Maua kwa muda wako.

MAUA SAMA: Karibu tena!

No comments