Kweli Duniani Wawili Wawili!


 Ni jambo la kawaida kuambiwa umefanana na mtu fulani, kwa sababu duniani wawili wawili kuna ambao hukutana na mikasa mbalimbali ikiwemo hata kupakaziwa kesi ambazo hawazijui labda kafanya mtu mwingine, lakini kwa kuwa kafanana naye msala unaweza kumuangukia yeye.

 

Ndivyo ilivyo hata kwa baadhi ya mastaa wetu hapa Bongo ambapo kuna baadhi wamekuwa wakifanana wenyewe kwa wenyewe, yaani staa kwa staa na kuna wengine hufanana na mashabiki zao, kiasi kwamba ukiwaangalia inakuwa ngumu sana kuwatofautisha. Twende tukawatazame mastaa hawa ambao wanafananishwa na watu wengine:

IRENE PAUL

Huyu ni msanii wa filamu nchini ambaye amewahi kutamba na muvi zake kama Love and Power, Kibajaji, Triple L, Mama Ntilie na nyingine nyingi, ni miongoni mwa mastaa ambao hupenda kufananishwa na watu mbalimbali.

 

Hivi karibuni amefananishwa sana na mrembo aliyefahamika kwa jina la Demetria Dyan McKinney ambaye naye ni msanii wa filamu na muziki kutoka nchini Marekani, kwa kweli ukiwaangalia utasema mapacha kwa jinsi sura zao zilivyofanana.

WEMA SEPETU

Ni mrembo aliyeshikilia Taji la Miss Tanzania mwaka 2006, mpaka sasa anatajwa kuwa ndio miss pekee ambaye bado nyota yake inazidi kung’ara kadiri siku zinavyozidi kwenda, licha ya changamoto zote alizopitia lakini hazikumfanya yeye kushuka kisanaa. Mrembo huyu naye amekuwa akifananishwa sana na mwanadada mmoja anayefahamika kwa jina la Tuerny, kuanzia sura, midomo mpaka kuongea.

NAIRATH RAMADHAN

Mwenyewe hupenda kujiita Nai kutokana na kazi ya u-video queen anayoifanya, watu wengi walianza kumtambua zaidi baada ya kunogesha katika wimbo wa Muziki ulioimbwa na msanii wa Bongo Fleva Darassa.

 

Mrembo huyu naye hayupo nyuma kwani mara nyingi amekuwa akijifananisha na mjasiriamali kutoka nchini Kenya, Huddah Monroe, kiasi cha kupelekea kujiita Nai Huddah na kweli ukiwatazama wanafanana sana.

RAJABU ABDUL

Ni msanii mkubwa wa muziki wa Bongo Fleva, wengi wanamfahamu kwa jina la Harmonize kutokana na kazi yake ya sanaa anayoifanya, miaka michache iliyopita alijitokeza kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Athuman Omary ‘Harmorapa’ akidai kuwa amefanana na msanii huyo hivyo anatamani kufanya naye kazi, ambapo Harmonize alimtolea nje.

 

Hata hivyo Harmorapa hakukata tamaa aliendelea kupambana na kuamua kujiita  Harmorapa ambapo mpaka sasa bado anaendelea na harakati zake za kimaisha.

ZARINAH HASSAN

Menyewe hupenda kujiita Zari The Boss Lady, ni mzazi mwenzake na staa wa muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, lakini pia ni mjasiriamali ambapo makazi yake yapo nchini Afrika Kusini, naye anaingia kwenye orodha ya mastaa waliofanana sana na mashabiki wao.

 

Miaka michache iliyopita alifananishwa na mrembo mmoja anayefahamika kwa jina la Martha Ainomugisha ambaye ni raia wa Uganda.

FAUSTINA CHARLES

Nandy ndiyo jina lake la kazi  ni msanii wa muziki wa Bongo Fleva ambaye kwa sasa anatamba na kibao chake cha ‘Do Me’ alichomshirikisha mchumba wake William Lyimo ‘Billnass’, miezi michache iliyopita alifananishwa na mrembo aliyefahamika kwa jina la Aiman ambapo picha zao zilisambaa sana mitandaoni. Ukimuangalia Aiman na Nandy unaweza kusema ni mtu na pacha mwenzake, wamefanana sana.

NASIBU ABDUL

Wengi hupenda kumuita mfalme wa muziki wa Bongo Fleva kutokana na jinsi alivyopambana kuhakikisha muziki wetu unafika mbali zaidi, lakini mwenyewe hupenda kujiita Diamond Platnumz, Mondi, Simba, Chibu au Dangote.

 

Amekuwa akifananishwa na watu wengi hasa mashabiki ambao hutokea kumpenda kwelikweli. Lakini hivi karibuni aliibuka kijana aliyefahamika kwa jina la Ismail na kuleta gumzo kubwa mitandaoni, jamaa kafanana na Mondi ile mbaya.

No comments