Ticker

6/recent/ticker-posts

Advertisement

'Hali yangu ya ulemavu wa ngozi imenikosesha ndoa'

'Hali yangu ya ulemavu wa ngozi imenikosesha ndoa'


 Baada ya kumaliza kusomea ualimu, Grace Chege alitamani sana kupata mume na kuanzisha familia. Alikuwa na matumaini tele lakini, kama anavyosimulia, hakujua kwamba safari ya kutafuta mume wa kufunga ndoa naye ingekuwa kama kuukwea mlima.

Baada ya muda, aligundua kwamba alikuwa anakabiliwa na changamoto zaidi kwenye safari hiyo kuliko wasichana wenzake.

Nini hiki kilichokuwa kikwazo kwake?

Kukurukakara za mapenzi

Grace alizaliwa akiwa na tatizo la ngozi lifahamikanalo kama ualbino.

Tangu akiwa mdogo, alitambua kuwa muonekano wake ni tatizo katika kufanya urafiki na watu wengine. Tatizo hilo liliendelea alipokomaa na kuwa mtu mzima.

Alikuwa na marafiki wa kiume ndio, lakini alipotaka wavuke hadi hatua hiyo nyingine na waanze kuchumbiana, walikuwa wakiyeyuka kama umande wakati wa jua.

"Nilitamani maisha ya ndoa kama mwanamke yeyote, kwa hivyo nilipomaliza shule ya sekondari na kuingia kwenye taasisi," anasema.

"Nilikuwa nawaona wenzangu wamekutana mara unasikia wanachumbiana na baada ya muda hao wameoana. Lakini nikawa nikishangaa nikwanini hawa wanaume niliokuwa nao walikuwa wananiogopa."

Grace alikuwa amejiwekea ahadi ya kutojihusisha na ngono hadi atakapofunga ndoa.
Maelezo ya picha,

Grace alikuwa amejiwekea ahadi ya kutojihusisha na ngono hadi atakapofunga ndoa.

Mwanamke huyu anasema kuwa pale kwenye taasisi alikuwa mchangamfu, na mwenye kujihusisha na shughuli za kidini kwa hivyo alitangamana na watu kila wakati .

Alisubiri angalau apate mwanaume amtongoze, lakini kana kwamba heshima ilizidi au kulikuwa na uoga fulani.

Kwa hio kwa miaka mitatu aliokuwa kwenye taasisi alisubiri hadi mwisho wa chuo.

Angalao alijiliwaza ya kuwa akipata ajira basi mchumba atapatikana tu.

Baada ya muda alibahatika kupata kazi kama mwalimu. Grace alikuwa amejiwekea ahadi ya kutojihusisha na ngono hadi atakapofunga ndoa.

Alihisi wanaume waliokuwa wanamwandama wakati akiwa pale shuleni walikuwa wana malengo tofauti kando na kumchumbia na kisha ndoa.

Kwa hivyo hakutilia maanani alipowagundua wanaume wa aina hio.

Kuchumbiana na mwalimu

Ila pale shuleni alipatana na mwalimu mwenzake ambaye walianza urafiki, Grace anasema kuwa walikuwa wamekubaliana kutoshiriki mapenzi kabla ya ndoa.

Kila kitu kilikuwa shwari kwake na mchumba wake, ila Grace anasema kuwa aligundua mabadiliko katika upande wa mpenziwe kwa mfano kujitenga kinyume na hapo nyuma ambapo wangeshirikiana kwa shughuli za kikazi na hata huduma za kidini nje ya kazi yao.

"Alibadilika tu na nikaanza kusikia tetesi kuwa alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na dada mwengine," anasema.

Grace Chege
Maelezo ya picha,

Grace aliambiwa na mchumba wake kuwa alikuwa amempa mimba mwanamke mwingine

Hakutilia maanani tetesi hizo na alijituliza kwa imani yake kwamba mwenzake alikuwa mwanaminifu kwake na kwa dini.

Mwanadada huyu anasema kuwa alipigwa na mshangao, pale yule mpenzi wake alipomuita pembeni siku moja, na kumueleza kuwa alikuwa amemtungisha mimba mwanamke mwengine na kwamba ingebidi afunge ndoa naye.

Grace alibaki mdomo wazi asijue la kufanya .

"Palepale nilihisi kuwa msimamo wangu wa kutofanya mapenzi kabla ya ndoa , ndio ulileta hali hii. Niliumia moyoni mwangu ila nilikubali msimamo wa aliyekuwa mchumba wangu," Grace anasema

Haikuchukua muda kwa mwanamke huyu kuondoka kwenye shule iliyokuwa imemuajiri kama mwalimu na kwenda shule nyengine alipoajiriwa.

Mapenzi ya kasi

Grace Chege

Akiwa katika pilkapilka za kikazi, alianza kuchumbiana na mwanamume ambaye alikuwa mwalimu kama yeye.

Uhusiano huu Grace anasema ulienda kwa kasi mno, ila ahadi yake ya tangu mwanzo ya kutoshiriki ngono kabla ya ndoa aliitilia maanani bado.

Mambo yalionekana kwenda shwari. Grace anasema kuwa mchumba wake pia alikubali hali yake ya kuwa albino na hakumbagua kwa chochote.

Pia alichukua hatua ya kumuelimisha kuhusiana na Albino ni nini.

Na kwa hio walielewana vyema.

Mwaka wa 2004 mwezi wa tano walikuwa wamekubaliana kuanza mchakato wa kufunga ndoa. Cha kwanza ni jamaa wa pande zote mbili kufahamiana na pia mahari kutolewa.

Lakini kabla ya sherehe iliyokuwa imepangwa kufanyika, mpenziwe Grace alimwandikia arafa kwenye simu yake ya mkononi.

Alimwambia kuwa alikuwa amesimamisha shughuli zote za kufunga naye ndoa.

Grace anasema kwamba alipigwa na butwaa na kuhisi kana kwamba ulimwengu wake ulikuwa umebadilika kabisa.

Tayari baadhi ya jamaa wa upande wa kwao na upande wa mpenziwe walikuwa wameelezwa kuhusu tarehe ya sherehe ya mahari na kadhalika.

Sasa Grace alishindwa amgeukie nani.

Mchumba wake Grace alimwambia kuwa anamuacha kwasababu ya hali yake ya ualbino
Maelezo ya picha,

Mchumba wake Grace alimwambia kuwa anamuacha kwasababu ya hali yake ya ualbino

Aliamua kuzungumza na mpenzi wake angalao aelewe sababu za yeye kuchukua hatua hizo za ghafla wiki mmoja tu kabla ya sherehe yao ya mahari.

"Nilipompigia simu hakuipokea, ila alituma ujumbe mfupi akihoji ni kwanini namsumbua. Niliamua kumpigia simu tena na kumsihi tukutane ili tutengane vyema ana kwa ana," Grace anakumbuka

Na je walipokutana mchumba wake alimpa sababu gani?

"Basi nilifunga safari kukutana naye, alinipa sababu za kuwa hali yangu ya kuwa albino, pamoja na kuwa baadhi ya jamaa zake walinikataa kutokana na hali yangu, kwamba hilo lilimfanya akate tamaa ya kunioa kama mke wake," anasema.

"Alisema kuwa alikuwa ana hofu ya kuishi na mwanamke wa muonekano kama huu kisa na maana watoto. Nilikata tamaa na kutamaushwa na jinsi mambo yalibadilika."

Grace aliambiwa na mchumba wake kuwa amemkataa kwasababu ya hali yake ya ualbino
Maelezo ya picha,

Grace aliambiwa na mchumba wake kuwa amemkataa kwasababu ya hali yake ya ualbino

Grace anasema kuwa ilibidi apige moyo konde na kumuomba mwenyezi Mungu kumpa ujasiri kupambana na matukio ya maisha.

Baadaye Grace alisikia kuwa yule mchumba wake alifunga ndoa na mwanamke mwingine.

Kuzaliwa na kujikubali kama Albino

Grace anasema kuwa kwao nyumbani walizaliwa ndugu watatu pamoja na yeye wakiwa na hali ya ualbino.

Mwanadada huyu anakiri kuwa wazazi wao waliwapenda na kuwakubali walivyo.

Hawakuwahi kusikia wamebaguliwa wala kutengwa kutokana na hali hiyo.

Grace anasema kuwa alifaulu kusoma hadi kiwango cha kuwa mwalimu kutokana na upendo wa dhati kutoka kwa baba na mama yao.

Grace aligundua kuwa mchumba wake alianza kubadilika kitabia na kuzanza kujitenga
Maelezo ya picha,

Grace amepata mafanikio mengi katika uongozi wa kanisa lake la Prebysterian church of East Africa (PCEA).

Lakini unyanyapaa mwingi ameuhisi wakati amekuwa mtu mzima anayetafuta mume.

Anasema kuwa moyo wake umevunjwa mara kadhaa na wanaume ambao waliogopa hali yake na kumuacha hoi.

Kweli anakiri ametimiza mengi, ikiwemo kuteuliwa kwenye baraza kuu la wazee kwenye parokia ya eneo la Banana Kaunti ya Kiambu kanisa la Prebysterian church of East Africa (PCEA).

Vilevile amekuwa mwalimu mkuu kwenye shule kadhaa nchini Kenya.

Grace Chege, ambaye kwa sasa ana miaka 50, umri ambao wengi huenda watamuona kama mzee, angali na matumaini ya kupata mchumba na hatimaye kufunga ndoa.

Post a Comment

0 Comments

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();