Asubuhi Hii! Kura Zaanza Kupigwa Zanzibar – Video


 Zoezi la upigaji kura ya mapema huko Zanzibar limeanza saa moja asubuhi. Kwa hii leo wanaopiga kura ni wa chache kwa sababu ya utaratibu uliopangwa. Mwanahabari wa BBC, Halima Nyanza yuko katika kituo cha upigaji kura katika Skuli ya Vikokotoni karibu kabisa na soko la Darajani.

 

Kura hii ya mapema ni ya kwanza kabisa kufanyika huko visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kura hii itawarahisishia watendaji ambapo wengi wao kesho Oktoba 28 watakuwa na majukumu ya kuhudumia wapiga kura ili kufanikisha tukio la kesho la upigaji kura.

 

Kutokana na kuwa mara nyingi huwa wanakosa nafasi ya kutekeleza haki yao ya kupiga kura ndio maana wakatengewa siku hii. Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Hamid Mahmod ametaja wale watakaohusika na kura hii ya mapema.

 

Wapiga kura watakaohusika na upigaji kura mapema ni kama ifuatavyo. Wasimamizi wa uchaguzi, pili wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupiga kura, askari polisi, wajumbe wa tume, watendaji wa tume, wapiga kura watakaohusika na ulinzi na usalama siku ya uchaguzi.

 

Bwana Mahmod amesisitiza kuwa wananchi hawatakiwi kwenda katika vituo vya kupiga kura isipokuwa tu kwa wale ambao orodha yao imewekwa vituoni kwa ajili ya kupiga kura ya mapema.

 

Aidha, kulingana na utaratibu uliopo ni kwamba sio vituo vyote vitakavyofunguliwa isipokuwa tu kwa vilivyoorodheshwa kama anavyofafanunua Mmwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Hamid Mahmod.

 

‘’Naomba ifahamike kuwa katika kila eneo la upigaji kura kutakuwa na kituo kimoja tu kitachopangwa kwa ajili ya kupiga kura ya mapema.

 

Kulingana na Mahmod vituo vingine vya kupiga kura vitafungwa na watendaji wa uchaguzi hawatakuwepo. “Pia vituo hivyo havitakuwa na masanduku ya kupiga kura wala kura zenyewe.” Kura zitakuwa kwa idadi maalum kuwatosheleza wapiga kura waliopangwa kupiga kura mapema tu.

No comments